Naibu wa Rais William Ruto ameombwa kushirikiana na mahakama ya ICC wakati wa kusikizwa kwa kesi dhidhi yake na mwanahabari Joshua Sang’.
Akizungumza mjini eldoret siku ya Jumatano, Mwenyekiti wa baraza la maimamu na wahubiri wa dini ya Kiislamu Kaunti ya Uasin Gishu, Abubakar Bini, alisema kuwa kesi hiyo itatupiliwa mbali iwapo Ruto ataonyesha ushirikiano wake na mahakama hiyo.
“Naibu rais asikatae kwenda ICC. Afuate utaratibu wa mahakama kama alivyofanya Rais Uhuru Kenyatta,” alisema Bini.
Bini alisisitiza kuwa Ruto asikubali kudanganywa na wanasiasa kwani kuna wale wanaotaka kumharibia jina.
“Ingawa wakenya wanataka kujiondoa katika mahakama hiyo, naibu rais asisikilize siasa zitakazo mharibia uongozi wake,” alisema Bini.
Aidha, alisema kuwa viongozi wa dhehebu mbalimbali wazidi kumwombea na kwamba mungu atamwongoza mwendesha mashtaka Fatou Bensuda kutupilia mbali kesi hiyo.
Aliomba kuwa wataofanya maombi kuhakikisha kuwa utaratibu wa maombi hayo yasiwe yale yatakayozua vurugu.