Seneta wa Kaunti ya Kisii Chris Obure amemuomba Mbunge wa Bobasi Stephen Manoti kutenga pesa za ustawi za maendeleo ya maeneo bunge (CDF) kusaidia Shule ya Wasichana ya Suguta.
Shule hiyo ni mojawapo ya shule zilizochaguliwa kuwa shule bora katika eneo hilo na kwa sasa mbunge huyo ameombwa kuisaidia na pesa za CDF ili iendelee kutoa elimu bora zaidi.
Akiongea na Waandishi wa habari siku ya Jumapili katika Shule ya Wavulana ya Nyamache, Seneta Obure alisema kuwa mbunge huyo yupo kwenye nafasi bora kusaidia shule hiyo na pesa ya CDF.
Obure alisema kuwa wakati alikuwa mbunge wa eneo hilo la Bobasi kabla ya kuwa seneta alipigania elimu bora katika baadhi ya shule katika eneo hilo huku Shule ya Wasichana ya Suguta ikiwa mojayapo.
Kwa sasa amemuomba mbunge Manoti kuendeleza mradi huo kwa kusaidia shule hiyo kama njia moja ya kuinua viwango vya elimu katika eneo bunge hilo.
“Namuomba mbunge wetu Manoti kushughulikia na kusaidia Shule ya Wasichana ya Suguta ili iweze kuendelea kutoa huduma bora ya elimu kwa wanafunzi kama shule hii ya wavulana ya Nyamache," alidokeza Obure.
Aidha, seneta huyo aliwaomba wakazi wa Bobasi kushirikina na mbunge huyo ili kuinua viwango vya maendeleo na kusema kuwa yeye wanaendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa eneo bunge la Bobasi ambao wote hutoka na Kisii Kaunti kwa jumla inaendelea kimaendeleo.