Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wawekezaji katika ukanda wa Pwani wameishinikiza serikali kuu kuzisajili ardhi za umma kupitia mfumo wa dijitali ili kuhakikisha kwamba unyakuzi wa ardhi unasitishwa.

Kulingana na wawekezaji hao, migogoro ya ardhi kila mara katika ukanda wa Pwani imechangiwa na wakazi kuuza ardhi zao kwa wawekezaji zaidi ya mara mbili, hatua ambayo inafaa kusitishwa ili kuwawezesha wawekezaji kufanya maendeleo.

Wakiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, wawekezaji hao wakiongozwa na mfanyibiashara amabye pia ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya My Space Property Mwenda Thuranira, walisema kwamba iwapo serikali itachukua jukumu la kutumia mfumo wa dijitali katika utaoaji wa hati miliki, basi mizozo ya ardhi inayoshuhudiwa itasitishwa.

“Tunaishiniza serikali kutumia mfumo wa dijitali kusajili ardhi za umma pamoja na utoaji wa hati miliki za ardhi kwani hatua hiyo itasaidia pakubwa katika kusitisha unyakuzi wa ardhi. Hatua hiyo pia itazuia wakazi kuuza ardhi zao zaidi ya mara mbili na kuzua vurugu,” alisema Thuranira.

Thuranira alisema kwamba hatua hiyo itawavutia wawekezaji wengi zaidi katika eneo la Pwani kufanya maendeleo pamoja na kubuni ajira kwa wakazi ili kuona kwamba uchumi unaimarika zaidi.

Mapendekezo ya wawekezaji hao yamejiri baada ya kushuhudiwa migogoro ya ardhi na kufurushwa kwa wakazi pamoja na nyumba zao kuvunjwa katika eneo la Dunga Unuse huko Changamwe, na Nguu Tatu katika eneo la Mwakirunge, Kaunti ya Mombasa.