Waendeshaji bodaboda katika vituo mbalimbali vilivyoko mjini Kisii wameiomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuweka vikingi karibu na vituo vyao kuzuia kugongwa na gari yanayopoteza mwelekeo.
Hii ni baada ya visa vya aina hiyo kushuhudiwa katika mji wa Kisii kila wakati. Mnamo siku ya Jumamosi, lori lilikosa mwelekeo na kuwagonga baadhi ya wahudumu wa bodaboda waliokuwa wanasubiri wateja katika kituo cha St Judes Kisii na kupelekea mmoja wao kunusurika kifo na kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii kwa matibabu kutokana na ajali hiyo.
Wakizungumza na Waandishi wa habari Jumapili, waendeshaji bodaboda hao wakiongozwa na mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda wa kituo cha Hema Felix Mokua, waliomba serikali ya Kaunti ya Kisii kujali maisha yao na kuwawekea vikingi kwa kila kituo chao kwani wamehofia maisha yao kuwa hatarini baada ya visa hivyo kuongezeka.
“Na wale madereva wa kusababisha ajali na kuwagonga waendeshaji bodaboda wanastahili kuchukuliwa hatua kali ya kisheria kwani wengi wa madereva hao mara nyingi hutoroka baada ya ajali,” alisema Francis Ogero, mwendeshaji bodaboda mwingine.