Mbunge wa Likuyani Enoch Kibunguchy amekariri kujitolea kwake kwenye vita dhidi ya ufisadi, akisema kuwa ni sharti ukome kwenye eneo bunge lake ili waweze kuafikia maendeleo wanayotarajia.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza ofisini mwake mjini Eldoret mapema Jumamosi, Kibunguchy alisema kuwa amepokea lawama nyingi kutoka kwa wananchi kuhusu maafisa wake haswa wanaoshughulikia kugawa fedha za kustawisha maeneo bunge nchini CDF.

Kulingana na wananchi hao, maafisa wanaogawa fedha hizo wamekuwa wakiwaitisha wananchi pesa ili washughulikiwe na kugawiwa fedha hizo.

Kwa maafisa hao na wengine wanaojihusisha na ufisadi, Kibunguchy amewaonya wajihadhari kwa kuwa chuma chao ki motoni.

“Ni sharti ufisadi ukomeshwe Likuyani, la sivyo, malengo yetu ya maendeleo hayataafikiwa,” alisema Kibunguchy.

“Wale watu wote ambao wajihusisha na ufisadi, uchunguzi unaendelea na watajipata pabaya. Wote tutawafuta kazi,” aliongeza.

Kibunguchy aliongezea kuwa eneo bunge lake kuorodheshwa nambari ya nchini katika maendeleo ni jambo lililomfisha moyo, akihoji kuwa ni sharti eneo bunge lake liwe nambari ya kwanza ama ya pili.

“Mbona tusiwe nambari moja? Ni sharti tujikakamue kurudisha hadhi yetu kama Likuyani,” alisema Kibunguchy.

“Nilipokuwa mjumbe wa Lugari, tulikuwa namba mbili, kwani ni nini kilifanyika tusirudi hapo?,” aliuliza.

Aidha, Kibunguchy amewataka viongozi wote kujitolea ili kustawisha mashinani, akisema kuwa ugatuzi umesaidia sana katika kuleta maendeleo mashinani.