Utingo watano wametiwa mbaroni katika kituo cha matatu cha Kikuyu kwa kuita abiria kwa sauti ya juu.
Akizungumza siku ya Jumanne, mkuu wa polisi katika eneo la Kikuyu Mutune Maweu alisema watano hao walitiwa mbaroni kwa kuita abiria kwa sauti ya juu ambayo ni kinyume na sheria.
Alisema kwamba ni hatia kwa wahudumu wa bodaboda na matatu kuita abiria kwa sauti ya juu.
Maweu alielezea kwamba hulka hiyo ilikuwa imenoga licha ya wahudumu hao kuonywa, na kusema kuwa wengi wa wale wanaovunja sheria hiyo si wahudumu halisi wa matatu bali ni wale wanaonuia kujaza gari ili walipwe.
"Nawaonya wahudumu wa matatu dhidi ya kuvunja sheria hii kwa kuita abiria kwa sauti ya juu. Tabia hii hushudiwa mara nyingi asubuhi na jioni. Nawashauri wenyekiti wa 'Sacco' waweze kuweka mikakati au sheria zao katika vituo vya matatu zitakazozuia hatia hii,” alisema Maweu.
Alieleza kwamba watano hao wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Kikuyu ambapo wanangoja kufikishwa mahakamani watakapo shtakiwa kwa kosa hilo.
Alisema kwamba maafisa wa polisi watahakikisha kwamba tabia hii imekomeshwa miongoni mwa wahudumu wa matatu.
Bwana Erastus Mwai, mmoja wa wenyekiti wa Sacco za matatu katika kituo cha matatu cha Kikuyu alisema kwamba kama Sacco walikuwa wametekeleza mikakati ili kuweza kuzuia uvunjaji wa sheria.
Alieleza jinsi walivyoleta vibao vya kuashiria gari inayobeba abiria ili kuzuia utingo kuvunja sheria hii.
Alisema kwamba watashirikiana na polisi ili kuweza kuhakikisha kwamba sheria inafuatwa na kuongezea kuwa watapiga marufuku hulka hiyo katika vituo vya magari.