Vijana katika eneo la Kabete wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kufuatia tangazo la zoezi la usajili wa kikosi cha ulinzi nchini mwezi huu.
Akizungumza katika mkutano wa vijana, Kiongozi wa kundi la vijana la Kabete Youth Progress Association (KYPA), Bwana Geoffrey Kirigwa alisema kwamba zoezi hilo liliangazia vijana.
Kirigwa alisema vijana katika eneo hilo hawajakuwa wakijitokeza kwa wingi katika zoezi hilo, na kuongezea kwamba zoezi za aina hii hazifai kuisha bila ya vijana kujitokeza kwa wingi.
Alisema kwamba hata wale waliojaribu mwaka uliopita wanafaa kurudi bali wasife moyo.
Mwenyekiti huyo alisema vijana wanafaa kuhakikisha wanajitokeza na stakabadhi zinazostahili kwa zoezi hilo bali wasijihusishe katika zoezi hili wakiwa na stakabadhi bandia.
Kirigwa alisema vijana wengi hujipata wakivunja sheria na kutiwa mbaroni wanapoenda katika zoezi hilo na vyeti bandia vya masomo.
Alihimiza vijana wasijihusishe na utoaji hongo bali waende katika zoezi hilo kwa haki na ukweli ili wanapopewa nafasi katika usajili huo, watumikie nchi kwa uzalendo.
"Zoezi za aina hii zinalenga vijana ambao ni wazalendo na wako tayari kutumikia nchi yao. Vijana wengi hapa hawajakuwa wakijihusisha na zoezi hilo jamba ambalo is nzuri. Hata hivyo, zoezi hilo litafanyika mwezi huu na nawahimiza vijana waweze kujitokeza kwa wingi na kwa haki," alisema Kirigwa.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Stephen Njenga, kijana katika eneo hilo, alisema kwamba atajaribu bahati yake na kuhusika katika zoezi hilo.
Alisema kwamba miaka miwili iliyopita alijaribu lakini hakufaulu na kuongezea kuwa himizo hilo lilimpa motisha na imani ya kujaribu tena mwezi huu.