Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya serikali kuanzisha hazina za kutoa mikopo nchini, vijana wa kaunti ya Kisii wameonekana kunufaika na pesa hizo na kujiendeleza kimaisha.

Mradi ambao umeonekana kupokelewa vyema na vijana wa kaunti hiyo ni ufugaji wa kuku ikilinganishwa na miradi mingine.

Ufugaji huo wa kuku unaendelea kufanya vyema na kuchangia pakubwa ukuaji wa uchumi wa taifa hili na vijana hao wamenufaika pakubwa.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu katika wadi ya Sensi kaunti ya Kisii, mwenyekiti wa kikundi cha ‘Maono Youth group’ Daniel Omweri alisema wanatarajia mradi huo utawapa faida ya kiasi cha hadi shilingi laki nne mwishoni mwa mwaka huu.

Vijana hao wa wadi ya sensi wametia fora kwenye maendeleo ya ufugaji wa kuku, hali ambayo imebadilisha pakubwa maisha yao na kupanua ajira miongoni mwa jamii ya mkisii na kupongeza serikali kwa hazina ilizoanzisha ili kunufaisha vijana kibiashara

Kikundi hicho kimeimarisha maisha ya wanachama wake, baada ya kuanzisha miradi mbalimbali inayowapa ajira dhabiti wakiwa pamoja katika vikundi hasa kupitia ufugaji wa kuku.

“Ikifika mwishoni wa mwaka huu au mapema mwaka ujao tutakuwa tumekadiria faida ya zaidi ya shillingi 400,000, ambayo itatokana na mauzo ya mayai, kuku na nyama ya Kuku,” alisema Omweri.

“Tumechagua viongozi mbalimbali ambo watakuwa wanasimamia vikundi vingine maana tunahitaji kugawanya vikundi kwa sababu hiki chenye tuko nacho kimekuwa kubwa Zaidi,” aliongezea.

Serikali imepongezwa kwa hazina iliyoanzisha, huku vijana hao wakisema walipata mkopo kutoka hazina ya Youth Enterprise Fund wakiwa vijana 12.