Wakili Steve Mogaka kutoka Kaunti ya Nyamira amewaomba vijana kuchukua vitambulisho na kujiandikisha kama wapiga kura ili kupata nafasi ya kuwachagua viongonzi wafaao ifikapo mwaka wa 2017.
Akiongeaa siku ya Jumapili katika eneo la Nyabite lililoko eneo bunge la Mugirango Magharibi, wakili Mogaka alisema kuwa kura ndio silaha muhimu ya kutumia kuhakikisha viongozi wazuri wenye wana ndoto ya kuwapelekea wakazi wa Kisii maendeleo.
Aidha, aliongeza kuwa kujiandikisha kwa wingi pia kutasaidia vijana kukabidhiwa pesa za Uwezo Fund na kufanyia biashara zao na hata pesa nyingi zitatoka kwa serikali kuu kuja kwa kaunti ili kufanya maendeleo pamoja na zile za ustawi maeneo bunge (CDF) ili kufanya maendeleo wakati wapiga kura wanajiandikisha kwa wingi.
“Nawaomba vijana kupata vitambulisho kwa wingi ili tuweze kuwachagua viongozi tunaowahitaji pamoja na kukabidhiwa pesa za Uwezo Fund ili mfanyie maendeleo,” alisema wakili Mogaka.
Wakati uo huo, Mogaka aliwaomba vijana walio na vitambulisho kuendelea kueneza habari ya umuhimu wa kuchagua viongozi ili wale hawajafanya hivyo wafanye bila taswishi wowote.
“Usajili wa wapigakura utakapoanza katika eneo hili, kila mtu ajisajili na wale ambao hawana vitambulisho nawaomba mujiandikishe kwa wingi,” aliongeza wakili Mogaka.