Vikundi vya akina mama na vijana kutoka eneo bunge la Bomachoge Borabu vimekabidhiwa shilingi milioni 12.6 kutoka hazina ya Uwezo Fund kama mikopo ili kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha.
Vikundi hivyo vilikabidhiwa pesa hizo siku ya Jumatatu katika uwanja wa shule ya msingi ya Ekerubo huku wakiagizwa kuzitumia kujiendeleza kupitia biashara na kupata faida.
Akizungumza siku ya Jumatatu wakati alipokuwa anawakabidhi pesa hizo kwa niaba ya mbunge wa eneo hilo, mkuu wa wilaya ya Kenyenya, Jaunga Mwajaunga aliwaomba vijana kutengeneza vikundi kwa wingi ili kupata fursa ya kutumia pesa za serikali kwa biashara tofauti na kupata faida kama njia moja wapo ya kupunguza hali ya umaskini.
Mkuu huyo alisemakuwa vikundi vichache vimejiandikisha kukabidhiwa pesa hizo ikilinganishawa na idadi ya watu katika eneo bunge hilo na kuwaomba vijana kujiandikisha kwa wingi.
Ikumbukwe kuwa hapo mbeleni vikundi hivyo vilikabidhiwa shilingi milioni 5.9 na kufikia sasa pesa ambazo wamezipata ni millioni 18.5 za kufanyia biashara ili kujinufaisha.
“Naomba vikundi vyote vilivyokabidhiwa pesa kuzitumia vizuri kutengeneza faida na msifanye mzaha na pesa hizo ili pindi mtakapozirudisha kwa hazina, muwe mumepata faida,” alisema Mwajaunga.