Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwataka Viongozi wa kisiasa eneo la pwani kuweka tofauti zao za kisiasa na kuungana ili kufanikisha maswala ya kimaendeleo, viongozi hao wameahidi kumuunga mkono Rais Kenyatta katika uchaguzi mkuu ujao.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama cha Republican Council (RC) Ibrahim Babangida, walisema kwamba watamuunga mkono Rais Kenyatta katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na juhudi zake za kuwaunganisha Wakenya pamoja na kufanikisha miradi ya kimaendeleo humu nchini.

Akizungumza mjini Mombasa baada ya kikao cha mazungumzo na wanachama wa chama cha TNA, Kaunti ya Mombasa siku ya Jumapili, Babangida alisema kwamba wameamua kujiunga na chama cha TNA chini ya mwavuli wa mrengo wa Jubilee Alliance na kumuunga mkono Rais kenyatta katika uchaguzi mkuu ujao.

Alisema kwamba atahakikisha viongozi wengine katika kaunti hiyo wanaungana.

“Sisi kama viongozi wa eneo hili tuko tayari kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu ujao na kuhakisha kuwa wakenya wamemchagua kwa mara nyingine. Rais Kenyatta ndiye kiongozi pekee anayeweza kuwaunganisha wakenya na taifa hili likasonga mbele kiamendeleo,” alisema Babangida.

Aidha, amesema kuwa viongozi hao watahakikisha kuwa wamewaunganisha viongozi wengine katika Kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani ili kuona kwamba wakazi wa Pwani wanakuwa na sauti moja ya uongozi.

“Wakazi wa kaunti hii na eneo zima la Pwani ni wenye sauti moja na sisi hatuoni kuwepo na pingamizi za kuwaunganisha wakazi pamoja na kumchagua Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2017,” aliongeza Babangida.

Tayari baadhi ya viongozi wakongwe wa kisiasa wamejiunga na mrengo wa Jubilee Alliance kutoka eneo la Pwani kupiga debe mchakato wa siasa kupitia mrengo huo ili kuona kwamba kiongozi wa taifa anarudi katika uongozi awamu nyingine ya pili.

Tayari mchakato wa kisiasa umeanza kupamba moto katika eneo la pwani, hususan maeneo ya mashinani kuwarai wakazi kuwachagua katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017.