Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa Baraza Kuu la Kiislamu, Sufi Supreme Council of Kenya, wamezindua mikakati ya kuzuru kaunti zote za Pwani ili kuwakinga vijana dhidi ya kujitosa katika itikadi kali.

Akilihutubia kongamano la kiusalama katika ukumbi wa Jubilee mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Sheikh Abdulakadir Al-Ahdan alisema kwamba ni sharti viongozi hao wa kidini waingilie kati ili kuwanasua vijana wadogo.

Sheikh Abdulkadir alisema kwamba baraza hilo litazidisha vikao vyake mashinani ili kutoa mwelekeo kwa vijana kuhusiana na msingi wa dini ya Kiislamu kama njia moja wapo ya kusitisha itikadi kali.

“Tumepanga kuendeleza vikao vya hamasa mashinani kuwaelimisha vijana athari za kujitosa katika itikadi kali na uhalifu, ili kufahamu vyema misingi ya dini ya Kiislam na kuishi katika hali njema na eneo letu kuwa salama,” alisema Abdulkadir.

Kiongozi huyo wa kidini ameitaka serikali kutumia mbinu ya majadiliano na kuwahusisha moja kwa moja viongozi wa kidini na wale wa kijamii ili kuwakinga vijana na maswala ya misimamo mikali.

“Tungeiomba serikali kutumia mbinu mbadala za kusitisha kukithiri kwa maswala ya itikadi kali ikiwemo njia ya mazungumzo, ili kuona kwamba eneo la pwani halikumbwi na changamoto za kisalama,” aliongeza Abdulkadir.

Viongozi hao wa dini ya Kiislamu chini ya baraza hilo wanaendeleza vikao hivyo vya kukabiliana na misimamo mikali na utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana eneo la Pwani.