Magavana wa kaunti zote za pwani pamoja na wabunge wamehimizwa kujenga vituo vya kurekebisha tabia ili kuwanasuru vijana wadogo waliyojitosa katika janga la utumizi wa dawa za kulevya eneo la pwani.
Kulingana na mkurugenzi wa bodi ya shirika la kupambana na utumizi wa mihadarati na vileo nchini Nacada Sheikh Juma Ngao vijana wengi wanaoshikwa wakitumia mihadarati hukiri kujitoa katika janga hilo lakini kutokana na uchache wa vituo vya kurekebisha tabia, vijana hao husalia katika masaibu yao.
Akiongea na wanabahari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Sheihk Ngao alisema kwamba ni jukumu la viongozi hao kushirikiana kujenga vituo hivyo katika kila kaunti na kuwachukua vijana hao katika vituo hivyo kwa matibabu.
“Ni jukumu la kila gavana kutenga shilingi milioni 100 na kila mbunge katika eneo bunge lake kutenga shilingi milioni 20 kupitia hazina ya CDF ili kutumika katika ujenzi wa kituo cha kurekebisha tabia cha Jumuiya ya kaunti za pwani,” alisema Sheikh Ngao.
Sheikh Ngao alisema kwamba ukanda wa pwani una zaidi ya vijana elfu 50 wanaotumia dawa za kulevya na kaunti ya Mombasa ikiwa na idadi ya waathiriwa elfu 23 hali ambayo inafaa kukabiliwa mara moja.
“Eneo la Pwani lina asilimia kubwa ya vijana waliyoathirika na utumizi wa dawa za kulevya. Kaunti ya Mombasa ndio inayoongoza kwa asilimia 23.3. Dawa zinazopatika katika Kaunti ya Mombasa ni aina ya Heroini, kokeini, bangi, Miraa na lazima hali hii kukabiliwa kikamilifu,” alisema Sheikh Ngao.
Mkurugenzi huyo amewashikiza viongozi hao kushirikiana na kuhakikisha kuwa ulanguzi na utumizi wa dawa za kulevya eneo la pwani linadhibitiwa na kubadilisha hali ya afya ya vijana hao waliyoathirika na mihadarati.
Mapendekezo ya mkurugenzi huyo yamejiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwahimiza viongozi wa kisiasa kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuwasaka walanguzi na watumizi wa dawa za kulevya pwani.