Share news tips with us here at Hivisasa

Hatua ya muungano wa upinzani wa Cord kutishia kumwondoa Rais Uhuru Kenyatta kwenye mamlaka imekashifiwa na viongozi wa Jubilee kutoka Kaunti ya Nakuru.

Akizungumza siku ya Jumatatu, Kaimu mwenyekiti wa chama cha TNA Kaunti ya Nakuru, Abdul Noor, alisema kuwa jambo hilo haliwezekani.

“Watu wanaoongea maombo ya kumwondoa rais kwenye mamlaka wajue alichaguliwa kikatiba na sio jambo rahisi wanavyofikiria. Huu ni mzaha na hiyo ni kuchezea nchi yetu ya Kenya. Mtu yeyote anayesema rais anafaa kuondolewa kwenye mamlaka ambayo alichaguliwa na wananchi ni mtu asiyetakia nchi yetu mema. Hatuwezi kukubaliana na mambo hayo,” alisema Noor.

Akiangazia swala la wanaomshutumu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ugatuzi Ann Waiguru kwa madai ya ufisadi, Noor aliwata wanaofanya hivyo kukoma kumpaka tope Waiguru kutokana na juhudi zake.

“Nchi hii ina sheria na bila shaka ni lazima sheria zifuatwe. Kama muungano wa Cord unaona Katibu Mkuu Waiguru ana makosa, watafute njia za kiutaratibu, kama ni kotini wampeleke. Hata hivyo, njia ya kwenda kumharibia jina hatuwezi kubali,” alisema Noor.

Matamshi yake yanafuatia madai ya upande wa upinzani kuwa Waziri wa Ugatuzi Ann Waiguru alihusika na ufisadi huku wakimtaka kujiondoa kwenye nafasi hiyo.