Share news tips with us here at Hivisasa

Askofu wa jimbo katoliki la Nakuru Maurice Makumba amewahimiza wadau wa elimu hapa nchini kufanya majadiliano yatakayopelekea mgomo wa walimu unaoendelea kwa sasa kufutiliwa mbali.

Akizungumza kwenye shule upili ya Upper Hill Nakuru siku ya Alhamisi, Askofu Makumba ambaye pia ni mwenyekiti wa tume inayoshughulikia maswala ya elimu na elimu ya kidini katika baraza la maaskofu wa kanisa katoliki hapa nchini KCCB, alisema elimu ni jambo la kutiliwa maanani na kutokana na hilo, linafaa kuchukuliwa kwa uzito.

“Kwa wakati huu ambao tunapitia nyakati za wasiwasi kutokana na mgomo wa walimu, tunaomba wale wote wanaohusika wakuje pamoja kujadiliana na kuafikia makubaliano yatakayoafikia suluhu mwafaka linalofaa wanafunzi na taifa hili kwa ujumla,” alisema Makumba.

Wito wa askofu huyu ni sawia na uliotolewa na kanisa katoliki tarehe Septemba 2, kupitia kwa taarifa.

Kwenye taarifa hiyo, kanisa katoliki lilionyesha kusikitishwa kwake na mgomo huo wa walimu unaolenga kushinikiza serikali kutekeleza agizo la mahakama la kuwapa walimu nyongeza ya kati ya asilimia 50 na 60 ya mishahara.

Ingawa kanisa katoliki lilishikilia kuwa ni sharti amri ya mahakama iheshimiwe, liliwataka walimu kuipa muda serikali kutekeleza hilo.