Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya shule ya upili ya kiadventista ya Nyanchwa iliyoko mjini Kisii kushika moto siku ya Jumanne na kusababisha hasara kubwa, wahisani wameombwa kujitolea kusaidia shule hiyo.

Wito huo umetolewa baada ya bweni ya shule hiyo kuchomeka, huku bidhaa vya wanafunzi zaidi ya 40 vikiteketea na kusababisha hasara kubwa. 

Akizungumza siku ya Jumanne katika shule hiyo, mwalimu mkuu Andrew Moindi alisema mali ya wanafunzi hao vikiwemo vitabu, godoro na blanketi vilichomeka, baada ya bweni hilo kushika moto wakati wanafunzi wakiwa darasani, na kuomba wahisani kusaidia shule hiyo ili kurejesha hali yao ya kimasomo ya kawaida .

Maafisa wa kuzima moto katika kaunti ya Kisii wakishirikiana na wananchi walifanikiwa kuzima moto huo, ingawa hadi sasa chanzo cha moto huo hakijabainika.

Mikasa ya moto imekuwa ikishuhudiwa katika shule mbalimbali katika kaunti ya Kisii, huku vyanzo vya visa hivyo vikiwa havijainika vyema. 

Mwalimu wa shule hiyo alisema hasara waliyoipata kama shule na wanafunzi ni kubwa zaidi, huku mali ya dhamana isiyojulikana ikiteketea. 

“Naomba tupewe usaidizi ili wanafunzi wapate malazi yao na wanunuliwe vitabu na bweni la shule lirekebishwe," alisema Moindi.