Wahudumu wa malori ya kubeba mizigo kutoka maeneo ya South Coast kuingia kisiwani Mombasa wamelalamikia hatua ya mamlaka ya huduma za feri nchini KFS, kupandisha ada ambayo magari hayo yanatozwa.
Akiongea katika kivuko cha Likoni siku ya Jumapili, mwenyekiti wa madereva hao Ahmed Abdi, alisema kuwa ada ambazo zinatarajiwa kuongezwa zitawavunja moyo wawekezaji ambao tayari wamekuwa na azmio la kuwekeza kwenye miradi ya uchukuzi.
Abdi aliwaomba wasimamizi wa KFS kuliangalia suala hilo upya na vile vile kuwahusisha washika dau ili kupata maafikiano ambayo yatawaridhisha wahusika.
“Sharti maamuzi muhimu kama hayo kuandaliwa wakati uchumi ni mzuri kwani biashara nyingi za uchukuzi ziliathiriwa tangu kutangazwe hatari ya magaidi. Wawekezaji ambao walikuwa wanachukuliwa mali yao mara tatu kwa mwezi sasa wanachukuliwa mara moja baada ya miezi miwili,” alisema Abdi.
Aliongezea, “Wahudumu wengi wa malori haya hawana njia nyingine mbadala mbali na ubebaji na usafirizaji wa mizigo kutoka kisiwani Mombasa kuenda maeneo ya Lunga Lunga na baadhi kuingia nchi ya Tanzania.”
Shirika la huduma za feri kwenye kivuko kikuu cha Likoni mjini Mombasa, kilitangaza wiki jana kuwa kitaongeza ada za magari yote yanayovushwa kwenye kivuko hicho kutoka ada zile za kawaida.
Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hayo ya feri, Bwana Hassan Musa, kwenye mkutano wa siku ya Ijumaa na washikadau wa shirika hilo, alisema kuwa imewabidi kufanya hivyo kwa sababu ya mahitaji ya shirika hilo kuboresha huduma.
Musa alisema wanatarajia kuleta feri nyingine mpya ili kuwafaa wanaotumia kivuko hicho, ambapo ada hizo zimeongezwa kwa asilimia 50 kwa kila gari kutegemea na uzani wa magari.