Idara ya ya hali ya anga katika Kaunti ya Mombasa ikishirikiana na ile ya masuala ya dharura, imewahakikishia wakazi kuwa imeweka mikakati ya kupigana na janga hilo la mvua ya El Nino, ambayo inatarajiwa hivi karibuni.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa idara hiyo katika kaunti hiyo, tayari kila sekta husika katika kaunti imejiandaa na wapo tayari kulikabili lolote ambalo litazuka kutokana na mvua hiyo.
Akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Mombasa, mkurugenzi huyo Lydia Kinoti aliwataka wakazi kuwa makini na kusaidia kuleta nafuu iwapo kutatokea shida yoyote ambapo alisema kuwa mashirika mbalimbali tayari yametangaza kujitolea kwao kwa kusaidia katika shughuli hiyo.
Ikumbukwe kuwa mashirika mbali mbali pamoja na idara husika zilikutana wiki jana kujadili suluhu la kukabiliana na mvua hiyo, ambapo mashirika kama Shirika la Msalaba mwekundu, na wawakilishi kutoka idara ya kukabiliana na majanga ya dharura kutoka Kaunti ya Mombasa yalitoa wito kwenye mashirika mengine kujitokeza ili kuona maeneo ambayo huathiriwa mara kwa mara yananusurishwa kutokana na makali ya mvua hiyo ya El Nino.
Baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na majanga ya gharika hasa nyakati za mvua nyingi ni pamoja na maeneo ya Majengo, Maweni, Kizingo, Likoni na eneo la soko kuu la Kongowea ambalo limekuwa likiathirika zaidi kila mara.