Mkuu wa idara ya fedha katika Kaunti ya Nyamira Jones Omwenga aliwarai wakazi wa kaunti hiyo kutembelea ofisi yake kuchukuwa mikopo ili waanzishe biashara na kujiendeleza kimaisha.
Wito huu umetolewa baada ya kusemekana kuwa watu wengi hawajaendea pesa hizo hadi sasa, jambo ambalo lilimlazimu Omwenga kuwaomba wakazi hao kuenda kukabidhiwa pesa hizo ili wajiimarishe na kujiinufaisha kibiashara kama njia mojawapo ya kuinua uchumi wa kaunti hiyo.
Akizungumza mnamo siku ya Jumatatu katika mji wa Keroka wakati kituo cha magari cha Keroka kilikuwa kinafunguliwa rasmi, Omwenga aliwaomba wakazi hao kutuma ombi la kukabidhiwa mikopo.
“Serikali yetu ilitenga pesa ambazo wananchi watachukua kama mikopo maana tunahitaji watu wajiendeleze na kuinua uchumi wa Kaunti yetu ya Nyamira,” alisema Omwenga, mkuu wa idara ya fedha katika Kaunti ya Nyamira.
Omwenga aliongezea kuwa, "Kiwango cha mkopo tunaotoa cha juu zaidi ni Sh300,000 na cha chini kabisa ni Sh40,000."
Aidha, Omwenga alisema kufikia sasa ni watu wachache wametuma maombi ya kukabidhiwa hizo pesa na tayari wamezikabidhiwa na wameanza kuzifanyia biashara.
“Muungano wa magari (Matatu Saccos) na waendeshaji bodaboda wakija watakabidhiwa mikopo kwani uchumi wa kaunti unainuliwa kupitia biashara kama hizi zenu,” alisisitiza Omwenga.