Mwakilishi wa wadi ya Bahati Peter Nderitu ametoa wito kwa wakazi wa Bahati kutopotoshwa na watu wenye malengo ya kisiasa, kwa madai kwamba serikali ya Nakuru haitekelezi maendeleo mashinani.
Bwana Nderitu alisema hayo wakati ambapo siasa za kampeni ya uchaguzi wa mwaka wa 2017 katika eneo bunge la Bahati zinapigwa sana kwenye mitandao haswa Facebook, huku kila mmoja akijaribu kuelezea ufanisi au hitilafu zilizoko kwenye serikali ya Nakuru.
Akiongea katika ofisi yake siku ya Jumatatu, Nderitu alisema ni mapema kuanza siasa au kupima ufanisi wa serikali ya sasa chini ya katiba mpya, licha ya kwamba imefanikiwa pakubwa kuleta maendeleo mashinani.
Kulingana na mwakilishi huyo wa wadi, uongozi wake umefanikiwa pakubwa katika kuleta maendeleo kama ya barabara, maji na kuweka taa za usalama kati ya mingine.
Nderitu alisema kuwa katika wadi yake ya Bahati yenye lokesheni saba, katika kipindi cha miaka miwili wamefanikiwa kuweka maji ya mifereji katika lokesheni nne za Karunga, Landimawe, Kamiruri na Chania.
Alisema wanapania kuweka maji katika lokesheni tatu zilizosalia kabla ya miaka miwili ijayo.
“Niliahidi kwamba nitawatua akina mama mzigo wa kubeba maji kwa mitungi. Ninapania kukamilisha hayo katika muda wa miaka miwili. Kwa sasa, NAWASCO inaendelea na mikakati ya kuweka mita kwenye mifereji tuliyoweka ambayo tayari ina maji. kwa hivyo, siasa za mitandao kwamba nimebagua watu wengine katika kuweka maji hazina misingi,” alisema Nderitu.
Mwakilishi huyo pia alikosoa watu wanaopania kupigania viti vya kisiasa katika eneo hilo wanaosemekana kutembea wakidanganya watu kwamba ndio wanawawekea umeme nyumbani mwao.
Alisema kuwa mradi huo wa umeme umefadhiliwa na benki ya dunia, kwa ushirikiano wa serikali kuu.
“Nani hajui hii ni kazi ya benki kuu ya dunia kwa ushirikiano na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta? Tuache siasa za kikabila, siasa za chuki, tuendeleze kaunti yetu na taifa letu," alisisitiza Nderitu.