Kijana mmoja kutoka Nyabiosi iliyoko Wiyala ya Kenyenya katika Kaunti ya Kisii, James Saisi amewata wakazi wa kaunti hiyo kukumbatia ufugaji wa sungura ambao alisema umefifia miongoni mwa wakazi.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 aliyekuwa akiongea siku ya Jumanne mjini Kisii, alishangaa kwa nini watu wameacha kufuga wanyama hao ilhali wana umuhimu katika jamii hasa katika masuala ya utafiti miongoni mwa wanafunzi wanaosomea taaluma za sayansi za utafiti na masuala ya wanyama kwa ujumla.
Alisema anatarajia kupata wanunuzi wa nyama na mkojo wa sungura hivi karibuni kufuatia kupata mtalii mmoja aliyemuahidi kumtafutia soko la nyama ya sungura.
Pia alisema mnyama huyo wa sungura huwa na nyama tamu na pia mkojo wake hutumiwa na baadhi ya watu kutoka nchi za kigeni kama dawa ya kutibu ngozi, na hivyo basi akawasihi vijana wenzake, wazee na akina mama kujaribu ufugaji huo wa sungura kwani kumekuwa na watu kutoka nchi ya China na Indonesia wanaohitaji maji ya wanyama hao.
Saisi alisema kuwa eneo la Gusii kwa jumla lina mazingira mazuri ya kuendeleza shughuli zozote za ukulima na ufugaji kwa hivyo hamna sababu yoyote kwa wakazi kuwa nyuma kimaendeo hata wakati nafasi ipo wazi ya kujiendeleza kwa kujikita katika masuala tofauti ya kilimo.
Aliwataka wakazi wanao nia ya kujiendeleza katika shughuli za kilimo katika kitengo cha ufugaji kuwa huru na kutembelea ofisi za idara ya kilimo katika Kaunti ya Kisii kupata ushauri madhubuti na wa kitaalamu kinachowafaa kwa kuimarisha ufugaji na kilimo kwa jumla katika kaunti hiyo ambayo inafahamika kwa kuzalisha mboga na matoke kwa wingi nchini.
Kijana huyo alidokeza kuwa atajitahidi kufuga wanayama hao kwa wingi na akaiomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuwapa msaada wa kifedha vijana ambao wana moyo wa kujiendeleza katika nyanja za kilimo na ufugaji.