Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wanaotumia kivuko cha Likoni, mijini Mombasa, wameipongeza serikali ya kaunti pamoja na shirika la huduma za feri KFS, kwa kuwahakikishia wakazi kuwa feri mbili zinatarajiwa kuwasili katika kivuko hicho na kuboresha huduma kwa wakazi hao.

Wakiongozwa siku ya Jumatatu na Bwana Iddi Mawengo ambaye ni mzee wa mtaa katika eneo la Shell Beach sehemu ya Likoni, wakazi hao walisema kuwa feri hizo zitakuwa na umuhimu mkubwa mno ikizingatiwa kuwa kumekuwa na visa vingi vya misongamano ambayo imeweza kusababisha maafa katika siku za nyuma.

Hatahivyo, Iddi alipendekeza kuwa shirika hilo sharti pia liweze kupanua sehemu za kupakia magari na kuingizia watu ili kuruhusu angalau feri tatu kupakia watu na magari kwa wakati mmoja, ikilinganishwa na sasa ambapo mara kwa mara feri mbili ndizo zaweza kutumika kwa pamoja.

"Ingekuwa bora shirika hilo kuwa na kitengo cha feri au mashua maalum za kushughulikia visa vya dharura kama vile magari ya ambulensi na wagonjwa, kwa sababu kumekuwa na visa vya wagonjwa kufia njiani kwa sababu ya kuchelewa kwa feri au hata mara nyingine baadhi ya feri kukwama kwa sababu za kiufundi,” alisema Mawengo.

Mawengo alisema kuwa sharti shirika hilo kufanya bidii zaidi kuhakikisha kuwa feri zao zinafanyiwa huduma na kurekebishwa ili kujiepusha na kuharibika kwa mitambo na kuleta zogo kati ya wakazi na shirika hilo.

Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo la KFS, Hassan Musa, feri hizo zinatarajiwa kupunguza msongamano wa watu na magari kama mojawapo ya harakati za kuimarisha huduma kwa watumiaji wa kivuko hicho.