Wakili Alfaxard Osoro kutoka Kaunti ya Nyamira amemuomba Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga kuimarisha usalama kuwahakikishia usalama wakazi wa kaunti hiyo.
Hii ni baada ya maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria na kuimarisha usalama katika kaunti hiyo nyakati za usiku kudaiwa kukoma, jambo mbalo wakazi wa eneo hilo wamesema limepelekea kuongezeka kwa uhalifu katika kaunti hiyo.
Akizungumza na Wandishi wa habari katika mji wa Nyamira siku ya Jumatano, wakili Osoro alisema wiki iliopita washukiwa wa wizi walimchoma mshale mkazi mmoja katika eneo la Ekerubo, eneo bunge la Borabu na kuiba ng’ombe wake ambao alisema hawajapatikana hadi sasa.
Aliongeza kuwa wengine walijeruhiwa vikali na wezi hao ambao wameonekana kuwashambulia wakazi wa kaunti hiyo, jambo ambalo limepelekea wakili Osoro kumwomba kamishna wa kaunti hiyo kuimarisha usalama kwa kuweka maafisa wa polisi nyakati za usiku katika sehemu mbalimbali jinsi ilivyokuwa hapo mbeleni ili kulinda wakazi wa kaunti hiyo.
“Namuomba kamishna wa kaunti ya Nyamira aweke usalama wa kutosha kwa wakazi wa kaunti hii kwani huenda wengi wakateseka na kupoteza maisha yao kufuatia visa vya wizi vinavyo kumbwa na majeruhi na vifo kila majambazi hao wanapovamia vijiji,” alisema wakili Osoro.
“Wiki jana ng’ombe waliibwa kutoka eneo la Ekerubo na mkazi akauwawa, kwa bahati nzuri ng'ombe wengine walipatikana katika eneo la Kepsengei na haya yote hufanyika kwa sasababu hamna usalama wa kutosha hapa Nyamira,” aliongeza wakili Osoro.
Aidha, wakili huyo Osoro alisema Kamishna Onunga asipoweka usalama wa kutosha watafikisha malalamishi yao kortini ili suluhu ya kudumu kuhusu usalama upatikane Nyamira.
“Hatuoni kama yale yaliowekwa kwenye mkataba kati ya kabila ya Kipsgis na Wakisii kama yanasaidia maana mwaka wa 2012 kabila hizo mbili ziliweka mkataba wa maelewano wa usalama katika mpaka huo, lakini wizi wa ng’ombe unaendelea kuongezeka kila kuchao,” alisisitiza Osoro.