Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Walimu kutoka eneo bunge la Nyaribari Masaba, Kaunti ya Kisii wameapa kukusanya sahihi za kumwondoa afisini Waziri wa Elimu Profesa Jacob Kaimenyi.

Walimu hao wamesema Profesa Kaimenyi hajatii agizo la mahakama la kuamuru walimu waongezewe mshahara.

Hii ni baada ya Wabunge kushindwa kumwondoa afisini kwa kutoajibikia kazi yake vilivyo haswa kwa kupinga nyongeza ya mishahara ya walimu.

Akizungumza siku ya Ijumaa na Waandishi wa habari afisini mwake iliyoko eneo la Masaba Kusini, mwenyekiti wa chama cha Knut wilayani Masaba Kusini Meshack Obonyo alisema walimu wataendelea kupambana hadi haki yao itimizwe kwa kuongezewa mshahara.

Aidha, Obonyo alisema watahimiza walimu wote nchini kukusanya sahihi ya kumwondoa afisini Waziri Kaimenyi kwa kutoajibikia kazi yake vilivyo.

“Tume ya kuajiri walimu nchini (TSC) iliwasilisha malalamishi ya walimu ya kutaka waongezwe mshahara kwa mahakama iliamuru kuwa walimu wanastahili kuongezwa mshahara. Baadaye Waziri Kaimenyi anapinga agizo hilo la mahakama. Hatutakubali na tutamwondoa afisini,” alisema Obonyo, mwenyekiti wa chama cha walimu tawi la Masaba Kusini.

Mwenyekiti Obonyo ametishia kuwa walimu wote nchini wataungana na kumwondoa Kaimenyi afisini kwa kukusanya sahihi.