Shirika la Sir Henry Foundation kwa ushirikiano na Chuo cha African International College limewafadhili wanafunzi 100 wa kidato cha nne kusomea kozi ya tarakilishi bila malipo.
Wanafunzi hao ambao wanaendelea kufanya mtihani wa kitaifa wa KCSE wilayani Kisii ya Kati wamechaguliwa rasmi kutoka shule mbalimbali ili kusomea kozi hiyo pindi watakapomaliza mitihani yao ya kitaifa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Kisii, afisa wa shirika hilo Nickson Nyakweba alisema waliamua kuwafadhili wanafunzi hao kusomea tarakilishi baada ya mitihani ya kitaifa kama njia moja ya kuwazuia kujihusisha na mambo ya ulevi na kuzembea nyumbani.
Kulingana naye, wanafunzi hao waliochaguliwa watapokea mafunzo bila kulipa ili kueneza taaluma hiyo na kuwawezesha vijana kujua mengi kuhusu tarakilishi.
“Tumeanzisha masomo ya tarakilishi hasa sehemu za mashinani na tuliweza kuwafadhili wanafunzi 100 wilayani Kisii ya kati. Tutaendelea kwenda sehemu zingine ili watu wajifahamishe na tarakilishi maana ni mengi yanapatikana kwa tarakilishi,” alisema Nyakweba.
Aliongeza, “Wanafunzi waliochaguliwa ni wale ambao walichukua nafasi ya kwanza hadi nafasi ya 10 katika mtihani wa mwigo na wale wanatoka familia maskini zaidi.”
Wakati huo huo, Nyakeba aliomba wazazi wote katika kaunti ya Kisii kuwaelimisha watoto wao na kuwapeleka kusomea kozi za tarakilishi kwani nyakati za hivi karibuni, mtu hatawezafanya lolote bila kujua maneno ya taraklilishi.