Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi 15 wa kidato cha nne walifikishwa katika mahakama ya Mombasa siku ya Alhamisi wakikabiliwa na shtaka la kupatikana na makaratasi ya mtihani wa Kiswahili wa KCSE.

Wanafunzi hao walikamatwa na maafisa wa polisi siku ya Jumatano wakiwa katika Shule ya upili ya Changamwe.

Walifikishwa mbele ya Hakimu Susan Shitubi kwa kosa hilo la kupatikana na maswali ya mtihani yanayofanana na mtihani wa kitaifa wa KCSE.

Wanafunzi hao walikanusha madai hayo wakisema kwamba kamwe hawajapatikana na maswali ya mitihani hiyo.

“Maswali tuliyokuwa nayo hayahusiani na mitihani wetu wa kitaifa wa KCSE. Yale makaratasi tuliyokuwa nayo ni makaratasi ya mazoezi ya mitihani na sisi hatujawahi danganya wala kuingia na makaratasi ya udanganyifu kwa chumba cha kufanya mithani,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Hakimu Shitubi aliwaonya wanafunzi hao dhidi ya kushiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa inayoendelea kote nchini, na kuamuru waachiliwe kwa dhamana ya Sh800,000 kila mmoja ama mdhamini wa kiasi sawia na hicho.

Kesi hiyo itaskizwa tena tarehe Novemba 26, 2015.