Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanafunzi kwenye Kaunti ya Kisii wametakiwa kuendelea kushiriki masomo kwa kusaidiana na wanafunzi wenzao walimu wanapoendelea na mgomo.

Akiongea katika mji wa Suneka siku ya Jumapili, katibu mkuu wa tume ya kutetea haki za walimu nchini Knut, tawi la Kisii Kusini, Charles Mokua, alisema kuwa wanafunzi wazidi kufanya masomo kibinafsi kwa kushauriana na wenzao au kuwahusisha vijana wengine ambao washamaliza masomo yao na wanaendelea kufanya taaluma kwenye vyuo na taasisi mbali mbali kwenye kaunti.

Katibu huyo, alishauri wazazi kuwa karibu na wanao na kuwapa msaada wa kimasomo unapohitajika, akisema kuwa mgomo wa walimu ambao unaendelea na unaanza rasmi siku ya Jumatatu kote nchini, haujulikani utakamilika lina ila tu watakapoongezewa hela wanazodai serikali.

Bwana Mokua aliwashauri wanafunzi wa darasa la nane na wale wa kidato cha nne ambao wanatarajiwa kufanya mtihani wa taifa mwishoni wa muhula huu, kutumia muda wao vizuri na kujiepusha na masuala tofauti kwani wao ndio wataathirika zaidi mgomo huo unapoendelea kote nchini.

“Kila mwanafunzi sharti awajibikie masomo na wale ambao wanatarajiwa kufanya mitihani ya kidato cha nne na darasa la nane wakae karibu na vitabu na kudurusu vitabu na kutafuta mwelekeo kwa vijana wengine ambao wanaweza kuwafaa zaidi wakati huu wa mgomo,” alisema Mokua.