Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Mombasa kimewahimiza wanawake kujitokeza na kuihamasisha jamii kufahamu umuhimu wa kudumusha amani.

Kulingana na mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Mombasa, Afia Rama, kukithiri kwa visa vya uhalifu na ugaidi kumechangiwa na ukosefu wa hamasa na ajiri kwa vijana miongoni mwa jamii mashinani hali ambayo imekuwa tishio kwa jamii.

Akizungumza na wanahabari afisini mwake siku ya Jumamosi mjini Mombasa, Afia alisema kwamba chama hicho kimeanza kuhamasisha jamii katika eneo nzima la Pwani ili kuona kwamba jamii inawashauri vijana jinsi ya kuepuka ushawishi mbaya na kujitenga na makundi ya kihalifu.

“Sisi kama akina mama tunawahimiza wanawake wajitokeza tuende kule mashinani na kuielemisha jamii pamoja na vijana jinsi ya kujiepusha na makundi ya kihalifu ambayo yanasababisha ukosefu wa usalama katika makazi yetu,” alisema Afia.

Aidha, alisema kuwa tayari kuna baadhi ya maeneo wamezuru katika kaunti za Pwani kueneza amani kutokana na kampeni ya amani waliyoanzisha katika kaunti zote za Pwani na lengo la kuimarisha usalama.

Afia aliwahimiza wakazi kuunga mkono juhudi hizo na kuwaleta pamoja wakazi ili kuona kwamba kila eneo la kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kwa jumla liko salama na shughuli za kibiashara zinafanyika bila pingamizi za kihalifu.

“Ni lazima kwa wakazi kuja pamoja na kushirikiana katika kufanikisha malengo haya. Tukiwa tunaishi kwa amani basi shughuli za kibiashara na uchumi wetu utaimarika mara dufu,” aliongezea Afia.

Mwenyekiti huyo aliahidi kuzuru hadi maeneo ya magharibi mwa Kenya kuwahamisha wanawake na jamii kwa jumla ili kuona kwamba amani inadumishwa.