Naibu chifu wa lokesheni ya Nyanguru kaunti ya Kisii Enock Omanwa amesema wananchi wengi, haswa wa kike katika eneo hilo hawana vitambulisho vya kitaifa, ili hali wamefikisha miaka ya kuwa na vyeti hivyo.
Akizungumza siku ya Jumanne na waandishi wa habari ofisini mwake iliyoko katika wadi ya Kiogoro, naibu chifu huyo alisema kulingana na uchunguzi uliofanywa na ofisi yake unaonyesha kuwa wazazi wengi wa kike hawana vitambulisho.
Hii ni baada ya wazazi wa kike kushindwa kuwasilisha stakabadhi za watoto wao ili kupata cheti cha kuzaliwa maana wengi hawana vitambulisho.
“Tumeanzisha mradi wa kusajili watu, mradi ambao unafanywa na maafisa kutoka divisheni ya Kiogoro maana tuligundua wazazi wengi wa kike hawana vitambulisho katika eneo hili la Kiogoro,” alisema Omanwa.
Usajili huo umeanzishwa kufanywa kwa siku tatu mfululizo katika eneo la Matibo, eneo lililoko lokesheni ya Nyanko.
“Kwa wale hawana vitambulisho pia huwa vigumu kwa kupata kibarua cha kufanya kwani haiwezekani kwa mtu kupatiwa kibarua kama hana kitambulisho, aliongeza Omanwa
Mradi huo wa usajili utawasaidia watu kutoka kata ndogo tatu kama vile Nyanguru, Rianyamwamu na Riamomanyi, huku akiomba watu kujitolea kwa wingi ili kupata vitambulisho na kupiga kura mwaka wa 2017 na hata kupata kibarua.