Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi katika kaunti ya Kisii wametofautiana na wazazi kutoka kaunti ya Nyamira kuhusu mgomo wa walimu ambao unaoendelea kote nchini.

Hii ni baada ya wazazi kutoka kaunti ya Nyamira, wakiongozwa na mwenyekiti wao Vincent Mbura kuunga mkono kuwepo kwa mgomo wa walimu hadi walipwe nyongeza yao ya mshahara, huku wazazi kutoka kaunti ya Kisii kupitia mwenyekiti wao Richard Ogembo kuomba walimu kusitisha mgomo huo na kurudi shuleni mazungumzo ya mshahara yanapoendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, Ogembo aliomba walimu kurejea darasani na kutayarisha wanafunzi kwa mitihani ya kitaifa mazungumzo yanapoendelea kuhusu kuongezwa kwa mshahara wao.

“Serikali ilisema haina pea za kuwaongeza walimu, mbona wasirejee darasani na kuwafundisha watoto mazungumzo mengine yanapoendelea? naomba walimu waonee watoto wetu huruma na kurejea darasani ili kuwafundisha,” alisema Ogembo.

Siku ya Jumapili, Mbura aliwaunnga mkonoo walimu waendelee kugoma, na kuomba serikali kuwalipa walimu la sivyo wataelekea mahakama kushtaki serikali ili kuwafidia wazazi kwa hasara ya karo wazazi wameipata.

Mgomo wa walimu unaendelea kuzua hisia mbalimbali na kuchipuka kwa maswali mengi hususani kama walimu watalipwa na ni lini watarejea darasani.