Abdirizak Hussein amechaguliwa kuwa katibu mtendaji wa chama cha walimu nchini KNUT tawi la Garissa kwenye uchaguzi wa kuwateuwa viongozi wa chama hicho uliofanyika jana.
Abdirizak Hussein alipata kura 225 na alimbwaga mgombea mwenza Ibrahim Atosh aliyepata kura 127.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Hussein aliiagiza serikali kutenga fedha za marupurupu kwa walimu wanaofanya kazi katika kaunti ya Garissa na maeneo mingine ya Kaskazini mashariki mwa nchi.
Hussein alisema kuwa matukio ya mwaka jana ya mashambulizi katika kaunti za Garissa, Mandera na Wajir yaliathiri pakubwa sekta ya elimu na kupelekea walimu wengi waliokuwa maeneo hayo kujiuzulu na wengine kuondoka.
"Maisha ya walimu wanaofanya kazi katika maeneo haya yamo hatarini na ningeiagiza serikali kuu kuwatengea walimu hao marupurupu iwapo watakumbwa na hatari yeyote ya kiusalama" Hussein alisema.
Hussein alisema kuwa kuwapa walimu hao marupurupu ndio njia pekee ya kutatua uhaba wa walimu maeneo hayo na kuwapa walimu motisha wa kutenda kazi.
"Marupurupu hayo yatawafanya walimu warejee na ningeiomba serikali iwache kuwashurutisha walimu na vitisho vya kuwapiga kalamu," Aliongeza Hussein.