Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff amewahimiza vijana mjini Mombasa kujihusisha na masuala ya michezo badala ya kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na hata kukubali kutumiwa na viongozi wa kisiasa.

Akizungumza siku ya Jumamosi katika uwanja wa Bomani mjini Mombasa wakati wa fainali ya kombe la Mvita lililoleta pamoja vilabu 20 kutoka eneo bunge la Mvita, Abdulswamad alisema michezo kama soka, raga na riadha hulipa vizuri iwapo mchezaji atajituma na kutumia talanta yake vizuri.

"Wachezaji wengi nchini wamefaidi pakubwa kwa kutumia talanta zao vyema, wanajitegemea na wamejiendeleza vizuri bila kujihusisha na visa vya wizi ama uhalifu. Tumia kipaji chako ujinufaishe, usisubiri kupewa na mtu," alisema kiongozi huyo.

Kauli yake iliungwa mkono na mwaniaji wa kiti cha naibu rais wa shirikisho la kandanda nchini FKF Twaha Mbarak aliyesema michezo ni kama ajira yeyote ile ambayo inafaa kuheshimiwa.

"Wachezaji wengi duniani wameajiriwa na vilabu na wanalipwa kila mwisho wa mwezi, hivyo wewe kama kijana ukitumia talanta yako vizuri utayaona matunda ya kipaji chako," alisema Bw Twaha.

Twaha vilevile alihimiza serikali kuwekeza katika michezo kwa kujenga viwanja vyenye hadhi ya kimataifa ili kusaidia kukuza vipaji vya vijana nchini.

Kombe la Mvita hudhaminiwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff kila mwisho wa mwaka na huleta pamoja zaidi ya vilabu 20 kutoka eneo bunge hilo ambapo mshindi hutia mfukoni shilingi elfu 100,000.