Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Biashara ya uchukuzi katika Kaunti ya Kisii imeonekana kunoga huku sherehe za krismasi na mwaka mpya zikiendelea kukaribia.

Abiria katika kaunti hiyo walisema imekuwa mazoea kwa wahudumu wa magari mjini Kisii kupandisha nauli bila kufuata utaratibu, haswa wakati wateja wanapoongezeka.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili mjini Kisii, abiria hao walisema wamelazimika kulipa nauli na bei ya juu katika maeneo mengi baada ya sherehe hizo kukaribia.

Abiria hao, wakiongozwa na John Nyangweso, waliwataka wenye magari kuzingatia kulipisha nauli ya kawaida kila msimu kwani maisha yamekuwa magumu kwa wengi kufuatia ongezeko la gharama ya maisha.

Waliomba vyombo husika kuwajibika kwa kuingilia kati na kuwasaidia wakati hali kama hiyo inapotokea kwani hali ya kuichumi imebadilika nchini.

Wasafiri hao walisema kuwa nauli inastahili kupandishwa iwapo bei ya petroli na diseli imetangazwa kupanda nchini, huku wakiongeza kuwa bei hiyo ilipunguzwa hivi majuzi kwa hivyo wahudumu wa magari hawapaswi kuongeza nauli.

“Hatuelewi kwanini wenye magari wanaongeza nauli bila kufuata utaratibu ufaao. Tunaomba nauli iwe kama kawaida na isipandishwe,” alisema Nyangweso

Aliongeza, “Tunaomba wahusika katika sekta ya uchukuzi kuingilia kati kuagiza wahudumu hawa kutoongeza nauli kwani bei ya mafuta haijaongezwa,” alisema Marion Nyakundi, abiria.