Baada ya ajali moja kuwaacha na majeraha mabaya Ijumaa asubuhi, abiria pamoja na wafanyabishara katika jiji la Mombasa wamewataka wahudumu wa magari kuwa macho na kukoma kupeleka magari kwa kasi hasa katika maeneo ya mizunguko, hali ambayo wanadai inaendelea kusababisha ajali katika jiji hilo.
Akiongea siku ya Ijumaa na mwandishi huyu, George Otieno, ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo, alisema kuwa madereva sharti wawe makini wanapokaribia maeneo kumewekwa mizunguko ili kujiepusha na kusababisha ajali.
Otieno aliwalaumu wahudumu wa matatu kwa kutotilia maanani maisha ya abiria wanaobeba kwa kushindana barabarani huku wakikimbilia pesa kwa tamaa ya kufika maeneo mna watu kwa haraka bila kuzingatia sheria za bararani.
Alisema hali hiyo ndio ilichangia ajali ya asubuhi kwenye barabara ya Nyerere/Moi mzunguko wa Fontanella, ambako abiria wote walikuwa ndani waliweza kuumia vibaya.
Naye Tulla Bulghani, ambaye ni mfanyabiashara wa jiji la Mombasa alisema kuwa haraka za madereva ndicho chanzo kikubwa cha ajali katika jiji hilo, na kuitaka idara ya trafiki kukaza sheria dhidi ya wanaopatikana na hatia za kuendesha magari kasi na kupuuza sheria za trafiki.
“Hawa madereva hawana hati za kuwakubalia kuingia barabarani na wengi wao ni vijana wadogo, huendesha magari haya mara nyingi hawafuatia sheria za trafiki na hupeleka magari kwa kasi wakitafuta kupata abiria vituo vya mbele mbele ili kumzuia mpinzani mwenza asipate mbele yake,” aliongeza Bulghan.