Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku msako dhidi ya magari ambayo hayafuati sheria za halmashauri ya uchukuzi nchini NTSA ukiendelea, abiria wengi katika Kaunti ya Mombasa wamelalamikia kupandishwa kwa nauli kutoka sehemu mbalimbali.

Abiria hao waliwalaumu wenye matatu kwa kuongeza nauli kuwa mara mbili zaidi kuliko nauli ya kawaida.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, abiria hao walisema kuwa wahudumu wa matatu wamechukua nafasi hiyo kuwadhulumu.

Abiria hao waliwataka wahudumu hao kupunguza nauli hiyo na kuiomba serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na halmashauri ya NTSA, kushirikiana na kuwanasa wale ambao wanaendelea kuongeza nauli kinyume cha utaratibu na sheria za trafiki.

Samson Kyalo, mkaazi wa Magongo, alisema kuwa alilipa nauli marudufu bei ya kawaida kwa kuwa matatu zilizokuwa zinahudumu siku ya Jumatatu zilikuwa chache.

Alisema kuwa wahudumu wengi waliogopa kuendesha magari yao lwa kuhofia kunaswa kwa kuenda kinyume cha sheria.

Fatuma Swaleh, mkaazi wa Likoni, alisema alilazimika kutembea kwa miguu kutoka mahali anakoishi hadi katikati mwa jiji la Mombasa, anakofanya biashara.

“Ilibidi nitembee kwa vile bei ya nauli ilikuwa juu na zingeweza kulipa kiwango hicho. Naiomba serikali kuchukua hatua ya kuwakamata wahudumu ambao wamekuwa na mtindo huo wa kuongeza pesa kila mara,” alisema Swaleh.

Wakaazi hao walitoa wito kwa idara ya trafiki pamoja na halmashauri ya NTSA kuhakikisha kuwa wale wanaongeza nauli wanatiwa mbaroni na kushtakiwa.