Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulitokea kizaazaa baada ya feri mbili zinazohudumu katika kivuko cha Likoni Jumatano mchana kugongana kwenye upande na kuzua mchecheto miongoni mwa abiria ambao walikuwa kwenye feri ya MV Likoni.

Kisa hicho ambacho kilihusisha feri ya MV Nyayo,  ambayo ilikuwa inaelekea kuegesha na kuanza kupakiza, na ile MV Likoni ambayo ilikuwa imebeba abiria ilijipata kwenye mgongano mkali baada ya feri ya MV Nyayo kuzidisha kimo na kupotoka wakati ilikuwa inageuka na kuwatia abiria hofu kwa kudhania kuwa feri ilikuwa na hitilafu kutokana na sauti kubwa iliyotokana na kugongana huko.

Kulingana na Sammy Mwapemba, ambaye alikuwa ameabiri feri hiyo ya Likoni, wengi wa abiria walipata mshtuko kwa kugongana huko na kudhani ilikuwa inazama.

“Mimi nilikuwa nimekaa kwenye upande wa juu na nikashtukia sauti ya mgongano nikadhani ni injini ya feri imetoa mlipuko na papo ilikuwa inayumba na watu wengine waliokuwa juu ya feri walianza kupiga kelele kwa kuhofia,” alisema abiria huyo.

Hata hivyo, ilichukua juhudi za mdhibiti wa feri hiyo kuwakanya abiria na kuwataka watulie, na kusema kuwa huo ni mgongano wa kimakosa na kuwa wako katika mikono salama.