Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulishuhudiwa hali isiyo ya kawaida katika kivuko cha feri eneo la Likono Jumatatu jioni, baada ya kusemekana kuwa mtambo wa feri moja ambayo ilikuwa inapakia magari pamoja na watu kuanza kutoa moshi mwingi mno na kushukiwa kuwa mtambo huo uliungua.

Feri hiyo, MV Harambee, ilikuwa inapakia watu pamoja na magari kutoka eneo la kisiwani ambapo inasemekana kuanza kukumbwa na tatizo hilo kabla ya abiria ambao walikuwa wameingia katika feri hiyo kutakiwa kushuka ili kuangaliwa kiufundi.

Akiongea na mwandishi huyu baada ya kisa hicho, Fatma Masheah, msafiri, alisema kuwa alikuwa ameingia kwenye feri hiyo ya Harambee, na muda mchache baadaye wakatakiwa kushuka kufuatia moshi kuzidi kutoka kwenye injini na kuwafanya wahudumu wa feri hiyo pamoja na mwendeshaji wake kuchukua hatua hiyo ili kuweka usalama wa abiria pamoja na watumizi kwa jumla.

“Sisi tuliona moshi ukiwa mwingi ambao ulikuwa ukitoka kwenye mtambo wa feri, kitu ambacho kilitufanya kushikwa na shaka na baadaye tukatakiwa kuondoka humo ndani kwa sababu ya usalama wetu,” alisema mama huyo.

Hata hivyo, kulingana na mmoja wa wahudumu wa wa feri hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina, ilikuwa shida kwenye injini ya feri ambayo ilisababisha moshi kuvuka kwa wingi hewani.