Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chama cha kutetea maslahi ya walimu Knut katika kaunti ya Mombasa kimepongeza juhudi za watahiniwa wa darasa la nane wa mwaka wa 2015 kwa kuorodhesha matokea bora zaidi ya mitihani ya KCPE.

Akizungumza katika afisi za chama hicho eneo la Changamwe, mjini Mombasa siku ya alhamis, katibu wa chama hicho kaunti ya Mombasa Dan Aloo alisema kwamba matokea hayo yameonyesha juhudi bora za walimu, wazazi na wanafunzi jinsi walivyoshirikiana kuboresha sekta ya elimu kaunti ya Mombasa.

Aloo alisema kwamba hakuna shule ya msingi kaunti hiyo iliyoorodhesha matokeo duni huku akisema kwamba kaunti ya Mombasa ni kati ya kaunti kumi na mbili zilizotajwa kutoshiriki udanganyifu wa mitihani na kuzidi kuwaonya wanafunzi kujiepusha na ouvu huo.

Katibu huyo wa Knut alihimiza ushirikiano mzuri baina ya wazazi, walimu na wanafunzi ili kutimiza malengo ya wanafunzi na kuahidi kushirikiana na wasimamizi wa shule za msingi kaunti hiyo.

Wakati huo huo, ameikosoa serikali kwa kuzembea kuwashughulikia walimu mahitaji yao akisema kwamba hatua hiyo inachangia shule zingine kutofanya vyema katika mitihani ya kitaifa nchini.

"Serikali ndio inachangia kuwepo na matokeo duni ya mitihani ya kitaifa ya KCPE kutokana na kutoshughulikia vyema maslahi ya walimu na tunaiomba serikali kuangalia kwa kina jinsi watakavyoimarisha sekta ya elimu ili watoto wetu wafanye vyema zaidi katika mitihani ya KCPE,"alisema Aloo.

Hata hivyo, wanafunzi 2, 709 walihusika katika udanganyifu wa mitihani hiyo ikilinganishwa na mwaka wa 2014 ambapo zaidi ya wanafunzi 1,702 walikosa matokeo yao kutokana na udanganyifu wa mitihani.