Biwi la simanzi lilitanda katika kijiji cha Kegogi kwenye eneo la uwakilishi wadi la Bomwagamo Kaunti ya Nyamira siku ya Alhamisi wakati wa maziko ya mkurugenzi wa masuala ya uajiri kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Francis Onyoni.
Akihutubu kwenye hafla hiyo, spika wa bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko alisema mwendazake alikuwa kiongozi mchapakazi na aliyewajibika katika shughuli zake.
"Mwendazake alikuwa mtu aliyejitolea kwenye kazi yake na kiongozi aliyewajibika kazini, na kwa kweli ni pigo kubwa kwetu na inashangaza," alisema Nyamoko.
Kwa upande wake Gavana wa Kaunti hiyo John Nyagarama alitoa ahadi ya kuajiri mtoto mmoja wa familia ya marehemu Onyoni ili kuziba pengo aliloliacha mwendazake.
"Nikiwa kiongozi wa serikali ya kaunti hii nitahakikisha kuwa mtoto mmoja wa familia ya Onyoni ambaye ametuacha amepata kazi kwenye idara yeyote kwenye serikali ya kaunti ili awasaidie ndugu zake, na hii itakuwa njia mojawapo ya kuziba pengo aliloliacha marehemu," alihoji Nyagarama.
Ikumbukwe marehemu, mwenye umri wa miaka 52, alikuwa mwalimu mkuu kwenye shule ya upili ya Nyansabakwa kabla ya kuteuliwa kuhudumu kwenye wadhifa huo aliohudumu afisini siku mbili tu kabla ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani kule Nairobi. .