Kamati ya bunge kuhusu uchukuzi na miundo msingi imesema kuwa asilimia 65 ya ujenzi wa barabara reli ya kisasa ya kuanzia Mombasa hadi Kampala nchini Uganda imekamilika.
Mwenyekiti wa Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu uchukuzi na miundo msingi imesema kuwa kabla ya mwaka ujao wa 2017 barabara hiyo itaanza kutumika ili kuafikia malengo ya ruwaza ya mwaka wa 2030.
Akiongea na wanahabari katika eneo la kwanza la ujenzi wa barabara hiyo ya reli ya kisasa katika Bandari Mombasa, Kamanda amesema kuwa reli hiyo ya kisasa itasaidia pakubwa katika masuala ya uchukuzi sambamba na kuimarisha sekta ya utalii na uchumi wa nchi.
Amesema kuwa baada ya kamati hiyo kukamilisha ziara yake ya kutembelea barabara hiyo itawasilisha repoti yake katika vikao vya bunge kujadili masuala muhimu yanayotaji kuafikiwa huku akisema kuwa tayari baadhi ya vifaa vya kukamilisha ujenzi huo vimewasili.
“Tumekuja kama kamati ya bunge kuhusu uchukuzi kuangalia shughuli ya ujenzi na kukusanya ripoti kisha tutaiwasilisha mbele ya bunge kujadili masula muhimu,” alieza Kamanda.
Hata hivyo kamati hiyo imeridhishwa na shughuli za ujenzi wa barabara hiyo na kampuni hiyo ya ujenzi kutoka Uchina na kuishinikiza serikali kuhakikisha kuwa shughuli hiyo ya ujenzi inakamilika kwa wakati mwafaka.