Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amewataka viongozi wanaowatumia vijana Mkoani Pwani kuvuruga amani na kuwahangaisha wananchi kukoma, na badala yake wawatafutie ajira ili waweze kujitegemea.

Akizungumza na vijana mjini Mombasa siku ya Jumanne jioni, Awiti, ambaye tayari ametangaza azma yake ya kuuwania ugavana wa kaunti ya Mombasa, alisema ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi kuwatumia vijana kwa manufaa yao badala ya kuzitatua changamoto zinazowakumba.

‘’Leo hii unawatumia vijana wa wengine kuzua kero ili ujifaidi, jiulize kesho kijana wako akitumiwa na mwingine utajihisi vipi? Ni jambo linaloshangaza sana,’’ alisema Awiti.

Aidha, Awiti aliwahimiza vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kwa njia isiyofaa, wakati huu ambapo joto la kisiasa la uchaguzi wa 2017 linapozidi kupanda, na badala yake wajihusishe na shughuli za ujenzi wa taifa zitakazowanufaisha katika maisha yao ya kila siku.

Ni mapema mwezi huu ambapo mshirikishi mkuu wa masuala ya usalama katika ukanda wa Pwani, Nelson Marwa, alimwonya mwanasiasa mmoja mjini Mombasa kwa madai ya kuwafadhili makundi ya vijana wa Wakali Kwanza na Wakali Wao kuwahangaisha wenyeji katika baadhi ya sehemu mjini humo.