Mbunge wa Nyali Hezron Awiti Bollo amewasuta viongozi wa kisiasa wanaowachochea vijana kuzua vurugu katika kaunti ya Mombasa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Bw Awiti alisema vijana wanafaa kuunganishwa pamoja na kuhamasishwa jinsi ya kujiunga na makundi mbalimbali ya kimaendeleo ili kujikimu kimaisha badala ya kuwahusisha na uovu.
Awiti alisema kuwa jukumu la viongozi ni kuhakikisha maswala ya amani yanaangaziwa vyema sambamba na kuwasaidia vijana kutekeleza miradi ya kimaendeleo mashinani.
Mbunge huyo wa Nyali alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wa kisiasa katika kaunti hiyo wanaowatumia vijana kuzua vurugu kwa misingi yao binafisi, akisema kuwa hatua hiyo inafaa kusitishwa mara moja.
"Tunawaambia viongozi wanaowachochea vijana kuvuruga amani katika eneo letu wakome mara moja kwani hatua hiyo haitasaidia kumwezesha kijana kujihusisha na maswala ya kimaendeleo na kuboresha maisha yake katika siku za usoni," alisema Awiti.
Kiongozi huyo aliahidi kuzuru mashinani na kufanya vikao vya hamasa kuhakikisha kuwa jamii na vijana wanafahamu vyema umuhimu wa kudumisha amani nchini.