Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amesema kuwa kila Mkenya ana haki kikatiba kuwania uongozi iwapo ana azma ya kuwasaidia Wakenya kimaendeleo na katika masuala mengine muhimu nchini.

Akiwahutubia wakaazi wa eneo bunge lake la Nyali siku ya Ijumaa, Awiti alisema kuwa yuko tayari kuwania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao, ili kuhakikisha kuwa anabadili uongozi ulioko kwa sasa kwani wakaazi wa Mombasa hawajatekelezewa majukumu yao halisi.

Awiti alisema kuwa mwananchi ndiye atakayeamua nani atamchagua wakati wa uchaguzi huo, huku akiwataka wapinzani wake waliotangaza kuwania kiti hicho cha ugavana kutangaza sera zao kwa njia ya amani na uiano.

“Ninaomba viongozi wenzangu kufanya kampeni zao kwa njia ya amani na uiano ili kutowagawanya Wakenya kwa misingi ya kisiasa na kikabila kwani wananchi ndio watu tunaowategemea katika kufanya mabadiliko ya uongozi,” alisema Awiti.

Wakati uo huo aliwasuta viongozi wenzake wanaosema kuwa hajafikia kiwango cha kuwania ugavana wa Kaunti ya Mombasa.

Alisema kuwa mchakato wa kisiasa na utangazaji wa sera kwa wananchi ndio utakaoamua nani anafaa kuwaongoza wakaazi wa Kaunti ya Mombasa.

Kwa sasa mchakato wa kisiasa katika Kaunti ya Mombasa umeanza kupamba moto huku viongozi mablimbali wakionekana kukimezea mati kiti cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa.