Share news tips with us here at Hivisasa

Tofauti za kisiasa baina ya gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama na viongozi wa vijana katika kaunti hiyo zinaendela kutokota baada ya vijana hao kumtaja gavana Nyagarama kama kiongozi asiye shughulikia mahitaji ya wakazi wa kaunti hiyo.

Akihutubu kwenye hafla ya mazishi kule Magombo siku ya Jumapili, mmoja wa viongozi hao Nyambega Gisesa alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo ina mazoea ya kutowapa nafasi za ajira vijana wa kaunti hiyo huku wakiishtumu wizara ya vijana kama wizara ambayo imekuwa ikipuuza matakwa ya vijana katika kaunti hiyo. 

"Uongozi wa gavana Nyagarama ni chukizo kwa wakazi wa kaunti hii kwa maana idadi kubwa ya vijana wamekuwa wakinyimwa nafasi za ajira, hali ambayo imesababisha wengi wao kuishi maisha ya umaskini huku wizara ya vijana ikikosa maono ya kuinua hali ya maisha ya vijana," alisema Gisesa. 

Kwa upande wake rais wa muungano wa vijana unaofahamika kama Youth Can, alishangazwa na jinsi serikali ya kaunti hiyo inavyopokeza kandarasi kwa vijana ilivyo kikatiba. 

"Kwa kweli sisi vijana tunafuatilia kwa undani jinsi shughuli za upokezaji kandarasi katika kaunti hii zinavyoendeshwa kwa maana baadhi ya wanakandarasi hupokezwa kandarasi kulingana na mahusiano waliyo nayo na gavana Nyagarama huku vijana wakiendelea kuumia ilhali tunafaa kutengewa asilimia 30% ya kandarasi ilivyo kikatiba," alihoji Maeche.