Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Kaunti Nchini Anthony Njaramba, ametoa shinikizo kwa Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyikazi wa Serikali SRC kuhakikisha kuwa kuna usawa katika malipo ya wafanyikazi.
Akiongea kwenye kongamano la biashara lililowaleta pamoja mawaziri kutoka wizara za kaunti mbali mbali za pwani nchini na wadau wengine katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Njaramba aliilaumu SRC kwa madai kuwa imeshindwa kusawazisha mishahara ya wafanyikazi wa umma.
Nyaramba, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Ufugaji katika Kaunti ya Mombasa, alitoa mfano wa makatibu wa wizara, aliodai kuwa wanapokea marupurupu ya juu ikilinganishwa na mawaziri, hali aliyoitaja kuwa ni ufujaji wa fedha za umma.
Wakati huo huo aliyapinga madai yaliyoenezwa katika mitandao ya kijamii kwamba mawaziri wa kaunti walitaka kuongezwa mishahara na kudai kuwa matamshi hayo yanalenga kuleta uhasama baina ya Tume ya SRC na mawaziri hao wa kaunti nchini.
“Sisi hatujasema kwamba tunahitaji kuongezwa misharahara bali tunataka usawa wa malipo ya wafanyikazi kutekelezwa. Kama tunavyoona, tume ya SRC inalenga kuhujumu haki za wafanyikazi hasa mawaziri wa kaunti mbalimbali nchini,” alisema Njaramba.
Kando na hayo, aliwataka wadau waliokutana katika kongamano hilo kubuni mfumo maalum utakaohakikisha ukusanyaji ushuru kwa njia za sawa ili kuepusha kuwatoza wafanyibiashara ushuru mara mbili.