Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali imeshinikizwa kufufua viwanda vyote vya umma vilivyofungwa katika eneo la Pwani na kubuni ajira kwa vijana na akina mama, ili kuwawezesha kujikimu kimaisha.

Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba alidai kuwa serikali inawakandamiza Wakenya kutokana na kukosa kuwepo nafasi za ajiri.

Aliitaka serikali kufufua kiwanda kwa Sukari cha Ramisi kilichoko katika kaunti ya Kwale, Kiwanda cha Korosho katika Kaunti ya Kilifi na kiwanda cha nyama nchini kama inazingatia maslahi ya Wakenya.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Bedzimba alisema kuwa hatua hiyo imechangia pakubwa kuwepo na ukandamizaji wa jamii, huku akisema kuwa hatua ya kumteua Waziri wa Madini nchini Dan Kazungu ni njama ya kuwadanganya Wapwani.

"Tunataka kuona serikali ikifufua viwanda vyote vya umma vilivyofungwa katika eneo la Pwani na kuwapa ajira vijana na akina mama ikiwa kweli inataka kubadilisha uongozi wa taifa hili. Haya mambo yao ya kutadanganya sisi Wapwani hatutakubaliana nayo,” alisema Bedzimba.

Mbunge huyo wa Kisauni amewataka wakaazi wa Pwani kuwa waangalifu wanapowachagua viongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017 ili kuhakikisha kuwa taifa hili linabadilika kimaendeleo hadi mashinani.