Mbunge wa Kisauni Rashid Bezdimba amewataka vijana kuhakikisha kuwa wako katika mstari wa mbele katika kuimarisha usalama kwenye mitaa wanamoishi.
Mbuge huyo alisema kuwa hatua hiyo itawavutia wawekezaji na kuwaepusha vijana dhidi ya kujihusisha na masuala ambayo yanahatarisha uwepo wa amani na utulivu.
Kiongozi huyo alisema kuwa kuimarisha usalama mitaani na katika miji, kutawavutia wawekezaji kuja na kukuboresha hali ya uchumi ya wakaazi wa maeneo husika.
Akiongea jijini Mombasa siku ya Jumapili, mbunge huyo alisema kuwa ni muhimu kwa vijana kutafutiwa njia mbadala za kujikimu kimaisha, kama mbinu za kujishughulisha vilivyo katika masuala ya kuendeleza maendeleo na kujipatia riziki katika njia za halali badala ya kuingia kwenye makundi haramu ya kuwapotosha.
“Usalama unaanza na sisi kama vijana bila kuweka imani yetu kila mara kwa maafisa wa polisi. Tukifanya hivyo, tutawavutia wawekezaji ambao watakuwa na nia ya kuwekeza humu mwetu,” alisema Bezdimba.
Kaunti ya Mombasa imekuwa ikibiliwa na visa vingi vya ukosefu wa usalama kwa muda mrefu, huku vijana wengi wakijiunga na makundi haramu ya kueneza itikadi kali, huku wengine wakiwa katika uundaji wa makundi ya kuhangaisha wakaazi mitaa.
Eneo la Kisauni limekuwa na visa vingi vya uhalifu ambapo wakaazi wengi wameomba idara ya polisi kuongeza doria katika maeneo hayo.