Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba ameunga mkono kauli ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Bedzimba alimtaja Joho kama kiongozi mkakamavu na mwenye msimamo wa uongozi bora kuliko uongozi wa sasa wa Rais Uhuru Kenyatta.

Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Malindi, Bedzimba alisema kuwa masaibu na kashfa mbalimbali zinazolimbikiziwa Joho ni kutokana na azimio lake la kuwania urais mwaka wa 2022.

Aidha, aliwataka viongozi wengine kuunga mkono azimio la Joho ili kiongizi wa taifa mwaka 2022 atoke eneo la mkoa wa Pwani.

Mwezi uliopita, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho alitangaza azimio lake la kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Joho alisema Mpwani anayo haki na uwezo wa kuwania kiti cha urais, hivyo kunahaja ya Wapwani kuungana na kuchukua uongozi wa nchi.

Joho aliwataka viongozi wa Pwani kumuunga mkono kwenye uchaguzi huo wa mwaka 2022 ili kupata nafasi ya kuongoza taifa hili na kuwa Mpwani wa kwanza kuongoza nchi.

Aidha, aliongeza kuwa yuko na uwezo wa kuongoza na kuboresha uchumi wa taifa hili iwapo atachaguliwa kuwa rais.

“Miradi iliyoanzishwa na serikali ya Jubilee sawia na ahadi za miradi ya maendeleo zilizotolewa na Rais Kenyatta wakati wa ziara yake hapa Pwani ni siasa. Wananchi hawapaswi kusherehekea kwani miradi hiyo ni haki yao kikatiba,” alisema Joho.

Aliwataka viongozi wa Pwani kutokubali kununuliwa na muungano wa Jubilee.