Sekta ya biashara mjini Mombasa inatarajiwa kuimarika kufuatia kukamilika kwa mradi wa kuweka taa mitaani ulioanzishwa na serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na kampuni ya umeme nchini, Kenya Power.
Mradi huo uliopewa jina 'Mwangaza Mtaani' ulizinduliwa na Rais Uhuru Kenyattam mwezi Septemba 2015 huku ukilenga kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuwawezesha wafanyabiashara kuendeleza shughuli zao hata nyakati za usiku.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Gavana Ali Hassan Joho alitaja kukamilika kwa mradi huo kama hatua kubwa iliyopigwa na serikali yake ili kuboresha usalama mjini humo na kuiniua sekta ya biashara.
"Taa ni kila kitu, wafanyabiashara sasa wanaweza kufanya biashara zao hata nyakati za usiku bila kuhofia usalama wao," alisema Bw Joho.
Joho vilevile aliipongeza kampuni ya umeme nchini Kenya Power kwa namna ilivyoshughulikia mradi huo kwa uwepesi.
Mradi wa 'Mwangaza Mtaani' umeigharimu serikali ya kaunti ya Mombasa shilingi bilioni 1.2 na sasa utawawezesha wenyeji kutekeleza shughuli zao mchana na usiku.