Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba Timothy Bosire ameipongeza shule ya upili ya wavulana ya Nyambaria, baada ya shule hiyo kuandikisha matokeo mazuri kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE mwaka jana.
Akihutubu shuleni humo baada ya matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana kutangazwa rasmi, Bosire aliipongeza shule hiyo kwa kuwa miongoni mwa shule zilizofanya vyema zaidi nchini huku akiiahidi kujenga maktaba ya kisasa shuleni humo.
"Nina furaha sana kwamba Shule hii ya Nyambaria imetuweka kwenye ramani ya kitaifa kwa kufanya vyema zaidi kwenye mtihani wa kitaifa KCSE, na natumai kuwa mtaendelea kutia bidii hata zaidi, na ndio maana nami pia nitahakikisha kuwa maktaba ya kisasa yenye thamani ya kima cha shillingi millioni 12 imejengwa humu shuleni," alisema Bosire.
Mbunge huyo aidha alisema kuwa maktaba hiyo itawasaidia wanafunzi kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba kupata huduma za masomo shuleni humo, hali ambayo itasaidia kuinua viwango vya elimu katika eneo hilo.
"Ni jambo la muhimu kwamba maktaba hiyo itajengwa katika shule hii ili shule zingine katika eneo hili kufika hapa ili kuona jinsi huduma za masomo zilivyo kwa maana tunataka kuona shule zote zikifanya vyema kwenye mitihani ya kitaifa," aliongezea Bosire.
Haya yanajiri baada ya shule hiyo kuandikisha matokeo mazuri kwa kupata wanafunzi 17 waliopata alama ya A 17, A- 69, B+ 91, B 57, B- 37 na 13 C+, huku kati ya wanafunzi 283 waliofanya mtihani huo, 236 kufanikiwa kupata alama zakuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu.